Luka 6
Suala juu ya siku ya Sabato
(Mat 12:1-8; Marko 2:23-28)
1 Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano, na wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke ya ngano, wakaondoa punje zake kwa mikono, wakala. 2 Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, “Mbona mnafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato?” 3 Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma jinsi alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa? 4 Yeye aliingia katika nyumba ya Mungu, akachukua ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu, akala na kuwapa wenzake. Haikuruhusiwa mtu kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani.” 5 Hivyo akawaambia, “Mwana wa Mtu ana uwezo juu ya Sabato.”
Mtu mwenye mkono uliopooza
(Mat 12:9-14; Marko 3:1-6)
6 Siku nyingine ya Sabato, Yesu aliingia katika sunagogi, akafundisha. Mle ndani kulikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kulia ulikuwa umepooza. 7 Waalimu wa sheria na Mafarisayo walitaka kupata kisa cha kumshtaki Yesu na hivyo wakawa wanangojea waone kama angemponya mtu siku ya Sabato. 8 Lakini Yesu alijua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Inuka, simama katikati.” Yule mtu akaenda kusimama katikati. 9 Kisha Yesu akawaambia, “Nawaulizeni, je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuyaangamiza?” 10 Baada ya kuwatazama wote waliokuwa pale, akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Naye akafanya hivyo, na mkono wake ukawa mzima tena. 11 Lakini wao wakakasirika sana, wakajadiliana jinsi ya kumtendea Yesu maovu.
Yesu anateua mitume kumi na wawili
(Mat 10:1-4; Marko 3:13-19)
12 Siku moja Yesu alikwenda mlimani kusali, akakesha huko usiku kucha akisali. 13 Kesho yake aliwaita wanafunzi wake, na miongoni mwao akawachagua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume: 14 Simoni (ambaye Yesu alimpa jina Petro) na Andrea ndugu yake, Yakobo na Yohane, Filipo na Bartholomayo, 15 Mathayo na Thoma, Yakobo wa Alfayo na Simoni (aliyeitwa Zelote), 16 Yuda wa Yakobo na Yuda Iskarioti ambaye baadaye alikuwa msaliti.
Yesu anafundisha na kuwaponya watu
(Mat 4:23-25)
17 Baada ya kushuka mlimani pamoja nao, Yesu alisimama mahali palipokuwa tambarare. Hapo kulikuwa na kundi kubwa la wanafunzi wake na umati wa watu waliotoka pande zote za Yudea na Yerusalemu na pwani ya Tiro na Sidoni. Wote walifika kumsikiliza Yesu na kuponywa magonjwa yao. 18 Aliwaponya pia wote waliokuwa wanasumbuliwa na pepo wachafu. 19 Watu wote walitaka kumgusa, kwa maana nguvu ilikuwa inatoka ndani yake na kuwaponya wote.
Heri na ole
(Mat 5:1-12)
20 Yesu akawageukia wanafunzi wake, akasema: “Heri nyinyi mlio maskini, maana ufalme wa Mungu ni wenu.
21 Heri nyinyi mnaosikia njaa sasa, maana baadaye mtashiba. Heri nyinyi mnaolia sasa, maana baadaye mtacheka kwa furaha.
22 “Heri yenu nyinyi iwapo watu watawachukia, watawatenga, watawatukana na kuwaharibieni jina kwa ajili ya Mwana wa Mtu. 23 Wakati hayo yatakapotokea, furahini na kucheza, maana hakika tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Kwa maana wazee wao waliwatendea manabii vivyo hivyo.
24 Lakini ole wenu nyinyi mlio matajiri, maana mmekwisha pata faraja yenu.
25 Ole wenu nyinyi mnaoshiba sasa, maana baadaye mtasikia njaa. Ole wenu nyinyi mnaocheka kwa furaha sasa, maana baadaye mtaomboleza na kulia.
26 Ole wenu nyinyi iwapo watu wote wanawasifu,
maana wazee wao waliwafanyia manabii wa uongo vivyo hivyo.
Kuwapenda maadui
(Mat 5:38-48; 7:12a)
27 “Lakini nawaambieni nyinyi mnaonisikiliza, wapendeni maadui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukieni. 28 Watakieni baraka wale wanaowalaani, na waombeeni wale wanaowatendea vibaya. 29 Mtu akikupiga shavu moja mgeuzie pia la pili. Mtu akikunyanganya koti lako mwachie pia shati lako. 30 Yeyote anayekuomba mpe, na mtu akikunyanganya mali yako usimtake akurudishie. 31 Jinsi mnavyotaka watu wawatendee nyinyi, watendeeni wao vivyo hivyo.
32 “Na ikiwa mnawapenda tu wale wanaowapenda nyinyi, je, mtapata tuzo gani? Hakuna! Kwa maana hata wenye dhambi huwapenda wale wanaowapenda wao. 33 Tena, kama mkiwatendea mema wale tu wanaowatendeeni mema, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi hufanya hayo. 34 Na kama mnawakopesha wale tu mnaotumaini watawalipeni, je, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wenzao ili warudishiwe kima kilekile. 35 Ila nyinyi wapendeni maadui zenu na kuwatendea mema; kopesheni bila kutazamia kurudishiwa, na tuzo lenu litakuwa kubwa, nanyi mtakuwa watoto wa Mungu aliye juu. Kwa maana yeye ni mwema kwa wale wasio na shukrani na walio wabaya. 36 Muwe na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma.
Juu ya kuwahukumu wengine
(Mat 7:1-5)
37 “Msiwahukumu wengine, nanyi hamtahukumiwa; msiwalaumu wengine, nanyi hamtalaumiwa; wasameheni wengine, nanyi mtasamehewa. 38 Wapeni wengine wanavyohitaji, nanyi mtapewa. Naam, mtapokea mikononi mwenu kipimo kilichojaa, kikashindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika. Kwa maana kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho atakachotumia Mungu kwenu.”
39 Akawaambia mfano huu: “Je, kipofu anaweza kumwongoza kipofu mwenzake? La! Wote wataanguka shimoni. 40 Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, lakini kila mwanafunzi akisha hitimu huwa kama mwalimu wake. 41 Kwa nini wakiona kibanzi jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako? 42 Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako,’ na huku huioni boriti iliyomo katika jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe! Toa kwanza boriti iliyomko jichoni mwako, na hapo ndipo utaona sawasawa kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako.
Mtu hujulikana kwa matunda yake
(Mat 7:16-20; 12:33-35)
43 “Mti mzuri hauzai matunda mabaya, wala mti mbaya hauzai matunda mazuri. 44 Watu huutambua mti kutokana na matunda yake. Ni wazi kwamba watu hawachumi tini katika michongoma, wala hawachumi zabibu katika mbigili. 45 Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka katika hazina bora iliyomo moyoni mwake; na mtu mbaya hutoa yaliyo mabaya kutoka katika hazina mbaya iliyo moyoni mwake, kwa maana mtu huongea kutokana na yale yaliyojaa moyoni mwake.
Wajenzi wa namna mbili
(Mat 7:24-27)
46 “Mbona mwaniita ‘Bwana, Bwana,’ na huku hamtimizi yale ninayosema? 47 Nitawapeni mfano unaofaa kuonesha alivyo yeyote yule anayekuja kwangu, akasikia maneno yangu na kuyatimiza: 48 Huyo anafanana na mtu ajengaye nyumba, ambaye amechimba chini na kuweka msingi wake juu ya mwamba; kukatokea mafuriko ya mto, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, lakini haukuweza kuitikisa, kwa sababu ilikuwa imejengwa imara. 49 Lakini yeyote anayesikia maneno yangu asifanye chochote, huyo anafanana na mtu aliyejenga nyumba juu ya udongo, bila msingi. Mafuriko ya mto yakatokea, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, ikaanguka na kuharibika kabisa!”
Luke 6
1 Now it came to pass on a sabbath, that he was going through the grainfields; and his disciples plucked the ears, and did eat, rubbing them in their hands.2 But certain of the Pharisees said, Why do ye that which it is not lawful to do on the sabbath day?3 And Jesus answering them said, Have ye not read even this, what David did, when he was hungry, he, and they that were with him;4 how he entered into the house of God, and took and ate the showbread, and gave also to them that were with him; which it is not lawful to eat save for the priests alone?5 And he said unto them, The Son of man is lord of the sabbath.6 And it came to pass on another sabbath, that he entered into the synagogue and taught: and there was a man there, and his right hand was withered.7 And the scribes and the Pharisees watched him, whether he would heal on the sabbath; that they might find how to accuse him.8 But he knew their thoughts; and he said to the man that had his hand withered, Rise up, and stand forth in the midst. And he arose and stood forth.9 And Jesus said unto them, I ask you, Is it lawful on the sabbath to do good, or to do harm? to save a life, or to destroy it?10 And he looked round about on them all, and said unto him, Stretch forth thy hand. And he did so: and his hand was restored.11 But they were filled with madness; and communed one with another what they might do to Jesus.12 And it came to pass in these days, that he went out into the mountain to pray; and he continued all night in prayer to God.13 And when it was day, he called his disciples; and he chose from them twelve, whom also he named apostles:14 Simon, whom he also named Peter, and Andrew his brother, and James and John, and Philip and Bartholomew,15 and Matthew and Thomas, and James the son of Alphaeus, and Simon who was called the Zealot,16 and Judas the son of James, and Judas Iscariot, who became a traitor;17 and he came down with them, and stood on a level place, and a great multitude of his disciples, and a great number of the people from all Judaea and Jerusalem, and the sea coast of Tyre and Sidon, who came to hear him, and to be healed of their diseases;18 and they that were troubled with unclean spirits were healed.19 And all the multitude sought to touch him; for power came forth from him, and healed them all.20 And he lifted up his eyes on his disciples, and said, Blessed are ye poor: for yours is the kingdom of God.21 Blessed are ye that hunger now: for ye shall be filled. Blessed are ye that weep now: for ye shall laugh.22 Blessed are ye, when men shall hate you, and when they shall separate you from their company, and reproach you, and cast out your name as evil, for the Son of man’s sake.23 Rejoice in that day, and leap for joy: for behold, your reward is great in heaven; for in the same manner did their fathers unto the prophets.24 But woe unto you that are rich! for ye have received your consolation.25 Woe unto you, ye that are full now! for ye shall hunger. Woe unto you, ye that laugh now! for ye shall mourn and weep.26 Woe unto you, when all men shall speak well of you! for in the same manner did their fathers to the false prophets.27 But I say unto you that hear, Love your enemies, do good to them that hate you,28 bless them that curse you, pray for them that despitefully use you.29 To him that smiteth thee on the one cheek offer also the other; and from him that taketh away thy cloak withhold not thy coat also.30 Give to every one that asketh thee; and of him that taketh away thy goods ask them not again.31 And as ye would that men should do to you, do ye also to them likewise.32 And if ye love them that love you, what thank have ye? for even sinners love those that love them.33 And if ye do good to them that do good to you, what thank have ye? for even sinners do the same.34 And if ye lend to them of whom ye hope to receive, what thank have ye? even sinners lend to sinners, to receive again as much.35 But love your enemies, and do them good, and lend, never despairing; and your reward shall be great, and ye shall be sons of the Most High: for he is kind toward the unthankful and evil.36 Be ye merciful, even as your Father is merciful.37 And judge not, and ye shall not be judged: and condemn not, and ye shall not be condemned: release, and ye shall be released:38 give, and it shall be given unto you; good measure, pressed down, shaken together, running over, shall they give into your bosom. For with what measure ye mete it shall be measured to you again.39 And he spake also a parable unto them, Can the blind guide the blind? shall they not both fall into a pit?40 The disciple is not above his teacher: but every one when he is perfected shall be as his teacher.41 And why beholdest thou the mote that is in thy brother’s eye, but considerest not the beam that is in thine own eye?42 Or how canst thou say to thy brother, Brother, let me cast out the mote that is in thine eye, when thou thyself beholdest not the beam that is in thine own eye? Thou hypocrite, cast out first the beam out of thine own eye, and then shalt thou see clearly to cast out the mote that is in thy brother’s eye.43 For there is no good tree that bringeth forth corrupt fruit; nor again a corrupt tree that bringeth forth good fruit.44 For each tree is known by its own fruit. For of thorns men do not gather figs, nor of a bramble bush gather they grapes.45 The good man out of the good treasure of his heart bringeth forth that which is good; and the evil man out of the evil treasure bringeth forth that which is evil: for out of the abundance of the heart his mouth speaketh.46 And why call ye me, Lord, Lord, and do not the things which I say?47 Every one that cometh unto me, and heareth my words, and doeth them, I will show you to whom he is like:48 he is like a man building a house, who digged and went deep, and laid a foundation upon the rock: and when a flood arose, the stream brake against that house, and could not shake it: because it had been well builded.49 But he that heareth, and doeth not, is like a man that built a house upon the earth without a foundation; against which the stream brake, and straightway it fell in; and the ruin of that house was great.